Saturday, December 31, 2016

BW. WASIA MAYA NA BI. LAILA MARTIN WAMEREMETA HOUSTON, TEXAS

Siku ya Alhamis tarehe 29/12 Bw. Wasia Maya kutoka mjini Houston , Texas aliamua kuachana na kambi ya makapera na kufunga ndoa na Bi. Laila Martin. Harusi hiyo ilifanyika nyumbani kwa Bw. Wasia na kuhudhuriwa na Watanzania wengi waishio katika jiji la Houston na miji ya jirani. Ijumaa ya tarehe 30/12 kulifanyika Nikka Dinner katika ukumbi wa Pakwan uliopo kwenye makutano ya barabara za HW6 na Beechnut . Pata picha za Harusi na Nikka Dinner hapa chini

Bw. Wasia na Bi. Laila siku ya ndoa yao
Maharusi wakiwa na sura za furaha Bw. Wasia na mkewe Bi. Laila
Bibi Harusi Bi. Laila

Bw. Wasia

Bi. Laila

Friday, December 30, 2016

DRC WAPINZANI WASEMA MAZUNGUMZO YALEGALEGA

Wapinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanasema mazungumzo ya namna Rais Joseph Kabila atakavyoondoka madarakani yanalegalega na yamkini yakasambaratika.
Kwa mujibu wa FĂ©lix Tshisekedi mmoja kati ya vinara wa upinzani, pande husika katika mazungumzo hayo zinakaribia kusambaratika kuliko kupata suluhisho.
Leo mazungumzo baina ya serikali na vyama vya upinzani chini ya upatanishi wa Kanisa Katoliki yamefanyika mjini Kinshasa. Jana Alhamisi makasisi wapatanishi walikutana na Rais Kabila pamoja na kiongozi mkongwe wa upinzani Etienne Tshisekedi ili kujaribu kufikia mwafaka.
Kwa mujibu wa mapatano yaliyopendekezwa, Kabila hatabadilisha katiba ili ashiriki katika uchaguzi mkuu mwakani. Aidha utawala wake wa mihula miwili ambao ulimalizika Disemba 19 utaongezwa hadi mwaka 2018.
Etienne Tshisekedi
Mazungumzo baina ya pande mbili yalikaribia kumalizika wiki jana ili kuandaa mazingira ya ukabidhianaji madaraka kwa amani kupitia mchakato wa demokrasia kwa mara ya kwanza tokea nchi hiyo ijinyakulie huru mwaka 1960. Hata hivyo kizingiti kikuu kimeripotiwa kuwa ni iwapo waziri mkuu atoke mrengo mkuu wa upinzani. Aidha kumekuwepo mvutano kuhusu Tume ya Uchaguzi ambayo wapinzani wanasema inaegemea upande wa serikali.
Watu 40 walipoteza maisha wiki jana mjini Kinshasa katika maandamano ya kutaka Kabila aondoke madarakani baada ya kuitawala nchi hiyo tokea mwaka 2001 wakati baba yake, Laurent Desire Kabila, alipouawa.